1 Thessalonians 5

1Sasa, kwa habari ya muda na nyakati, ndugu, hamna haja kwamba kitu chochote kiandikwe kwenu. 2Kwa kuwa ninyi wenyewe mwajua kwa usahihi ya kuwa siku ya Bwana inakuja kama mwizi ajapo usiku. 3Pale wasemapo kuna “Amani na usalama”, ndipo uharibifu huwajia ghafla. Ni kama utungu umjiavyo mama mwenye mimba. Hawataepuka kwa njia yeyote.

4Lakini ninyi, ndugu hampo kwenye giza hata ile siku iwajie kama mwizi. 5Kwa maana ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi siyo wana wa usiku au wa gizani. 6Hivyo basi, tusilale kama wengine walalavyo. Bali tukeshe na kuwa makini. 7Kwa kuwa wanaolala hulala usiku na wanao lewa hulewa usiku.

8Kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, tuwe makini. Tuvae ngao ya imani na upendo, na, kofia ya chuma, ambayo ni uhakika wa wokovu wa wakati ujao. 9Kwa kuwa Mungu hakutuchagua mwanzo kwa ajili ya gadhabu, bali kwa kupata wokovu kwa njia ya Bwana Yesu Kristo. 10Yeye ndiye aliyetufia ili kwamba, tukiwa macho au tumelala, tutaishi pamoja naye. 11Kwa hiyo, farijianeni na kujengana ninyi kwa ninyi, kama ambavyo tayari mnafanya.

12Ndugu, twawaomba muwatambue wale wanaotumika miongoni mwenu na wale walio juu yenu katika Bwana na wale wanao washauri. 13Tunawaomba pia muwatambue na kuwapa heshima katika upendo kwa sababu ya kazi yao. Muwe na amani miongoni mwenu ninyi wenyewe. 14Twawasihi, ndugu: muwaonye wasio kwenda kwa utaratibu, watieni moyo walio kata tamaa, Wasaidieni walio wanyonge, na muwe wavumilivu kwa wote.

15Angalieni asiwepo mtu yeyote anayelipa baya kwa baya kwa mtu yeyote. Badala yake, fanyeni yaliyo mema kwa kila mmoja wenu na kwa watu wote. 16Furahini siku zote. 17Ombeni bila kukoma. 18Mshukuruni Mungu kwa kila jambo, kwa sababu hayo ndiyo mapenzi ya Mungu kwenu katika Yesu Kristo.

19Msimzimishe Roho. 20Msiudharau unabii. 21Yajaribuni mambo yote. Mlishike lililo jema. 22Epukeni kila mwonekano wa uovu.

23Mungu wa amani awakamilishe katika utakatifu. Roho, nafsi na mwili vitunzwe pasipo mawaa katika kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. 24Yeye aliyewaita ni mwaminifu, naye ndiye mwenye kutenda.

25Ndugu, tuombeeni pia. 26Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu. 27Nawasihi katika Bwana kwamba barua hii isomwe kwa ndugu wote. 28Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.

Copyright information for SwaULB